TAMKO LA EDWARD NGOYAI LOWASSA KUHUSU HATMA YAKE KISIASA


Ndugu watanzania wenzangu awali ya yote nitoe shukrani zangu za dhati kwa namna mlivyoniunga mkono nikiwa ndani na nje ya CCM nikitafuta kuteuliwa na hata nilipokuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema Kwa mwavuli wa UKAWA. Hapa natoa pongezi za kipekee kwa Mwenyekiti Mbowe, Maalim Seif, James Mbatia na UKAWA kwa ujumla kwa kunipa heshima hiyo.

Pili, nimeamua kuwatangazia rasmi watanzania wenzangu adhma yangu ya kustaafu siasa na kubaki kama mshauri kwa vyama vya upinzani nchini vinavyounda UKAWA. Naamini historia yangu itanakiliwa kwa kuongoza mapinduzi ya kidemokrasia na kujenga hamasa ya kutosha miongoni mwa wananchi walio wengi hususani vijana kuyataka mabadiliko, na kuwabana viongozi wao katika uwajibikaji. Hatukuweza kwenda Ikulu, lakini nina uhakika tumetuma ujumbe kwa viongozi wazembe kwamba watanzania sio watu wa kuchukuliwa mzaha.
Tatu,nakiri zipo kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi huu, kama mkutano wangu na waandishi wa habari ulivyosema, sikubali matokeo yaliyotangazwa na tume. Lakini sitapenda kuingiza nchi yetu kwenye matatizo na machafuko. Hivyo nawaomba wafuasi wangu tuwe watulivu tukisubiri yanayojiri. Hata hivyo natambua kwamba Dkt. Magufuli ni kiongozi makini, nimewahi kufanya naye kazi katika awamu ya tatu na ya nne anazo sifa za kiuongozi zenye kujibu wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa Taifa letu katika kipindi hiki. Sisi hatukuwa na shida nay eye, bali mfumo mbovu wa CCM. Namuomba sana akatimize ahadi zake kwa wananchi bila kupuuza walioniunga mkono, na atambue kwamba tumeshapanda mbegu ya mabadiliko ambayo itaendelea kuchipua na kuwa imara, hivyo amekalia kuti kavu na uchaguzi ujao kama asipowatumikia watanzania basi awe tayari kuachia dola.
Mwisho, namkumbusha kuwa dhamana ya urais ni shughuli nzito hasa kwa Taifa ambalo lina changamoto nyingi kama letu. Kwa wale marafiki zangu wa zamani wa CCM tusijengeane chuki kwa yaliyotokea kwani niliamua kuitafuta haki yangu sehemu nyingine. Kwa wale wana Mabadiliko wenzangu, nawaambia Aluta Continua, tutumie bunge kama sehemu ya kuonyesha watanzania na kuanza kuwaletea mabadiliko tuliyoyahubiri.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Africa.

Edward N Lowassa.
29.10.2015

Unknown's avatar

Author: aggreywillis

See my 50 cents contribution to humanity as a founder of https://www.mactkenya.org Book publication on: https://www.morebooks.de/store/gb/book/condemning-women-and-babies-to-graves/isbn/978-3-8473-7888-4